Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika Mkutano wake wa kawaida robo ya kwanza Kwa mwaka wa fedha 2024/25 uliofanyika Novemba 14,2024 limempongeza Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajabu Magaro kwa usimamizi mzuri wa Miradi sambamba na ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza katika Baraza hilo Mhe Diwani wa kata ya Nyamalimbe Mhe Jeremiah Ikangala amesema Mkurugenzi anapaswa kuendelea kutiwa moyo kwa kuwa usimamizi wa Miradi ya Maendeleo unaonekana pamoja na ukusanyaji na matumizi ya Mapato ndani ya Halmashauri. "Tuendelee kumtia moyo Mkurugenzi ili kasi aliyo nayo katika usimamizi wa Miradi na ukusanyaji wa mapato iendelee ili Halmashauri isonge mbele" amesema Mhe Ikangala.
Katika taarifa yake Kwenye Baraza hilo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndg Karia Rajabu Magaro ametoa rai kwa Waheshimiwa Madiwani kuendelea kutoa ushirikiaono katika usimamizi wa Miradi ya Maendeleo katika kata zao ili Miradi hiyo iendelee kukamilika kwa wakati na kuwanufaisha Wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg. Karia Magaro akiwasilisha taarifa ya utendaji mbele ya baraza la madiwani
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Charles Kazungu amewataka Madiwani kuendelea kusimamia vema miradi inayo tekelezwa kupitia Fedha za Serikali kuu na Mapato ya ndani ili Miradi hiyo ikamilike kwa wakati. " Tusimamie Fedha za Miradi na niwatake Saruji ambazo ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji inazitoa tupange Mikakati mapema ili zisiharibike zilete tija kwenye kazi tulizokusudia" amesema Mhe Kazungu.
Vile vile Mhe Kazungu ameilekeza ofisi ya Mhandisi wa Halmashauri kukamilisha ramani na BOQ kwa wakati ili kasi ya Miradi isisimame”Nitoe rai kwenu tuongeze kasi ili tuweze kutekeleza miradi yetu ya maendeleo.”amesema Mhe Kazungu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kupitia mapato ya ndani imetoa mifuko 100 ya saruji kwa kata zote 37 za Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kuendelea kuchochea shughuli za maendeleo ndani ya Halmashauri. “Niwaombe waheshimiwa Madiwani kuendelea kutoa vipaumbele kwenye maeneo yanayokumbwa na maafa ili kuyanusuru kwa haraka huduma za kijamii zisisimame” ameongeza Mkurugenzi.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji amesihi Madiwani kuendelea kuwahamasisha wananchi kuwa na vikundi na kujiandikisha ili kupata mikopo ya asilimia 10 ambapo halmashauri ina jumla ya shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya kukopesha vikundi.
Jumla ya kiasi cha Shilingi Bilioni 2.4 kimekusanywa katika robo ya kwanza ambacho ni sawa na asilimia 28 ya mapato yaliyotarajiwa kukusanywa kwa mwaka.
Akihitimisha mkutano huo Mhe Kazungu amewataka waheshimiwa madiwani na wataalam wa Halmashauri kila mmoja kusimama kwenye nafasi yake ili kuendelea kudhibiti mapato ya Halmashauri huku akiwasisitiza madiwani hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi.
“Tuendelee kukusanya kwenye vyanzo ambavyo vipo chini ili kufikia malengo mapema na haraka na yeyote atakayekwamisha swala la ukusanyaji wa mapato sitamvumilia”amesema Mhe Kazungu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa