Na: Hendrick Msangi.
DC Cornel Maghembe apokea taarifa ya maagizo ya kamati ya siasa Wilaya ya Geita juu ya Miradi inayotekelezwa na Halmashauri za Wilaya
Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama cha Mpinduzi (CCM) katika kutekeleza majukumu yake wilayani Geita.
Kamati ya Siasa ilifanya ziara ya kukagua Miradi mbalimbali ndani ya Halmashauri hizo na kutoa maagizo kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya na Mji ili kuhakikisha malengo ya kiutendaji yanatimia.
Katika taarifa hizo zilizosomwa na Wakuu wa Idara katika Halmashauri, zimeeleza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi inayoendelea , miradi iliyo kamilika na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji na ukamilishwaji wa miradi kwa wakati.
Miradi iliyotolewa maelezo kwa mujibu wa maagizo ya kamati hiyo ya Siasa Wilayani humo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya madarasa, barabara, vituo vya afya, miradi ya machinjio, maji safi na salama pamoja na vikundi vya kijasiriamali vinavyoendesha shughuli katika Halmashauri hizo za Wilaya.
Akipokea taarifa hiyo, Mhe. Maghembe aliwataka watendaji wote kutekeleza wajibu wao ili kutimiza madhumuni ya chama cha Mapinduzi katika kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi.
" Tujisahihishe tunapokesea ili tuéndelee kufanya vizuri katika kutekeleza Miradi ambayo serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa fedha nyingi katika Halmashauri zetu na pia Wakurungezi fedha zinapoingia hakikisheni zinapelekwa kwenye miradi kwa wakati" alisema Maghembe.
Naye Mwenyekiti wa chama cha Mpinduzi (CCM)- Wilaya ndugu Barnabas Mapande ambaye aliongoza kamati hiyo ya Siasa katika kukagua Miradi mbalimbali ndani ya Halmashauri hizo, aliwataka Wakurungezi hao kusimamia maelekezo katika Utendaji na fedha zinazotolewa na Serikali Kuu.
" Kuwepo na ushirikiano Kati ya mafundi na wahandisi ili kuepuka dosari ndogo ndogo zinazojitokeza katika kutekeleza Miradi ambayo serikali inatenga fedha nyingi" alisema Mapande.
Akiendelea kutoa maoni yake juu ya maagizo yaliyotolewa na kamati ya siasa Wilayani Geita, Mapande alitoa maagizo kuhusu mradi wa Kokoto ambao unaendeshwa na kikundi cha Wanawake Mazoea kilichopo kata ya Nyawililwa kufuatiliwa upya ili mradi huo uwe na tija kwa kuhakikisha kunakuwepo na mashine za kuleta mawe, upasuaji na hata kupeleka kwa wateja ili kikundi hicho kiweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuzalisha kipato.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa CCM -wilaya, Katibu wa Umoja wa CCM -Wilaya, Mbunge wa Jimbo la Geita, Wakurungezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Mji pamoja na wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali kutoka Halmashauri hizo.
Aidha Mhe. DC Maghembe aliishukuru serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali Wilayani Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa