Na:Hendrick Msangi
WANANCHI wa Kata ya Nkome Halmashauri ya Wilaya ya Geita wamesisitizwa kujenga utamadini wa kuchangia pato la Taifa ili kuendelea kuijenga halmashauri kwa kuendelea kulipa tozo zinazotakiwa kwa kila biashara wanayoifanya pamoja na kujenga utamaduni wa kuendelea kuisimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao ili kumuunga mkono Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yameelezwa Machi 22, 2024 wakati Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba alipofanya ziara kwenye Kata ya Nkome kusikiliza kero na changamoto za wananchi wa kata hiyo ambayo wananchi wengi wa kata hiyo hujishughulisha na shughuli za uvuvi.
Wananchi wa Kata ya Nkome wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba kwenye mkutano wa hadhara ambapo kero mbalimbali za wananchi hao zilipatiwa majibu. Wananchi hao walisisitizwa kutokukaa na kero muda mrefu kwani serikali ya awamu ya sita ipo kuwasikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili.
Wananchi walipata fursa ya kueleza kero zao kwa Mkuu wa Wilaya ambapo baadhi ya kero walizo lalamika mbele ya Mkuu wa Wilaya ni pamoja na wingi wa michango mashuleni ikiwa ni michango ya mitihani na chakula huku wanafunzi wasiochangia kurudishwa nyumbani, wananchi kuuziwa nyumba zao na madalali pasipo amri ya mahakama, tozo za dagaa na samaki kwa wavuvi, magari ya abiria kutokufika kituo cha mabasi, mikopo ya vikundi vya ujasiriamali pamoja na kaya zinazonufaika na mfuko wa Tasaf wahusika wakidai kutokupata fedha hizo.
Akijibu kero hizo katika Mkutano mkubwa wa hadhara, Mhe Komba alikemea tabia ya uchangishaji wa michango mashuleni ambayo haijapata kibali kutoka serikalini.”Nimarufuku kwa shule zetu kuwa na michango ambayo ni holela,na ambayo haijapata kibali cha serikali kutoka ofisiya Mkuu wa Wilaya.” Alisema Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akizungumza na wananchi wa Kata ya Nkome alipofanya ziara kwenye kata hiyo kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua ikiwa ni agizo la Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wananchi wasikilizwe kero zao na kuzitatua.
Kuhusu swala la Lishe, aliwataka wazazi na walezi kutambua kuwa ni wajibu wao kuhakikisha watoto wanapata lishe wawapo shuleni kwa kufanya makubaliano kwani ni jambo la lazima shuleni. Mh Komba alikemea tabia ya kuwafukuza au kuwaadhibu watoto shuleni kwa sababu wazazi wao hawajatoa hela za chakula bali kuwataka walimu kuwafuatilia wazazi na walezi wao ili watoto wapate chakula kwa kipindi wawapo shuleni.
Akizungumzia swala la wananchi kuuziwa nyumba zao na madalali, Mhe Komba alikemea tabia hiyo na kusema kumekuwa na tabia za madalali wasio kuwa na amri ya mahakama kupiga mnada nyumba za wananchi.
Kilio cha wananchi kutoka kaya masikini ambao wamekuwa wakinufaika na fedha za mfuko wa TASAF kilimfikia Mkuu wa Wilaya ambapo alitoa maelekezo kwa waratibu wa mfuko huo wa kunusuru kaya masikini kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua wenye sifa na wasio na sifa za kupewa fedha hizo ili kuepuka malalamiko kwa wananchi kwani malalamiko mengine ni kukosa elimu kunakopelekea wanachi hao kulalamika.
Akitolea majibu kero ya mikopo kwa wajasiriamali, Mkuu wa Wilaya aliiagiza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kutoa maelekezo kwa watendaji wa kata na vijiji kufanya mikutano ya wananchi ili kutoa elimu juu ya fedha zinazoletwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi, pamoja na kuwasaidia wananchi kutengeneza vikundi ambavyo vitaorodheshwa ili kuweka uwazi wa fedha iliyotolewa na vikundi vilivyo nufaika na fedha hizo kufahamika na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akiwasikiliza wananchi katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika kata ya Nkome. Pamoja na kusikiliza kero zao, Dc Komba aliwataka wananchi hao kujenga utamadini wa kuchangia pato la Taifa ili kuendelea kuijenga halmashauri kwa kuendelea kulipa tozo zinazotakiwa katika biashara zao
Ili kuendelea kutatua kero za wananchi , Mhe Mkuu wa Wilaya alitoa maagizo kwa watendaji wa kata kuwa na dawati la malalamiko linalotembea kuwasikiliza wananchi ili kusogeza huduma jirani na wananchi kwani zipo kero ambazo zinaweza kutatuliwa katika ngazi ya kijiji au kata. “Watumishi nendeni mkawasikilize wananchi katika maeneo yao ili kushughulikia kero zao, tumeajiriwa ili kuwatumikia wananchi” alisema Mhe Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akipokea taarifa ya mradi wa kituo cha mabasi kata ya Nkome kilichojengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri kiasi cha Tshs. 79,000,000 Ambapo kiasi cha Tsh. 29,900,000 kilihamishwa TARURA kwa ajili ya ujenzi wa Barabara km 1 kutoka Nkome centre hadi stendi na kusawazisha eneo la stendi na kiasi kilichobaki Tsh. 49,100,000 kilitumika kujenga miundombinu ya stendi ikiwa ni ujenzi wa choo matundu 6 na vibanda 2.
Mwisho Mkuu wa Wilaya aliwashukuru wananchi wa Kata ya Nkome kwa kujitokeza kwa wingi kwenye Mkutano huo na kuwataka wasikae na malalamiko muda mrefu huku akiwasisitiza kushikamana na viongozi wao ikiwa ni pamoja na kuwa kuwa na utamaduni wa kuchangia kwenye mapato ya Halmashauri ili kuiwezesha halmashauri kufanya shughuli za maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa