Halmashauri ya Wilaya ya Geita, imefanya uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto –PJT-MMMAM leo Februari Mosi, 2024.
Uzinduzi huo umefanyika makao makuu ya Halmashauri - Nzera ambapo Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndugu Karia Rajabu Magaro, amesema uzinduzi huo umefanyika ngazi hiyo ya Halmashauri yakiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ambapo alielekeza programu hiyo izinduliwe ngazi zote kuanzia Taifa, Mkoa hadi Halmashauri.
Mkurugenzi Rajabu Magaro amesema uzinduzi huo ni mwendelezo wa baada ya uzinduzi ngazi ya Mkoa tarehe 21 septemba, 2023 na ngazi ya Taifa Desemba,2021.
Amesema program hiyo inalenga kukabiliana na kutokomeza changamoto zinazoonekana kuwa ni kikwazo cha “Hatua sahihi za ukuaji timilifu wa mtoto kimwili, kiakili na kijamii”.
“umri unaolengwa na program hii ni kuanzia umri wa miaka sifuri hadi miaka nane ambapo kwa mujibu wa tafiti za kisayansi imeonesha kuwa huo ndiyo umri nyeti wa kumtengeneza mtoto aliye bora au mtoto aliyedhaifu kimwili, kiakili na kijamii” alisema Karia.
Na kuongeza kwamba katika umri huo ubongo wa mtoto hupokea kile kinachoingia na mwili kujengwa kutokana na kile unachopatiwa.
Mkurugenzi Karia ametaja maeneo makuu matano ya msisitizo kwa ajili ya kuyazingatia wakati wa utekelezaji wa programu hiyo ambayo ni uzingatiaji wa huduma za afya bora kwa mtoto na mama ambapo kwa kufanya hiyo ni kutimiza adhma ya lengo namba 3 ya Maendeleo endelevu ya Dunia inayozungumzia Afya bora.
Eneo la pili, Mkurugenzi huyo amesema ni lishe ya kutosha kwa mtoto na mama mzazi kuanzia akiwa mjamzito, na la tatu ni Malezi yenye Mwitikio.
Maeneo mengine amesema ni fursa za ujifunzaji wa awali na eneo la tano ni ulinzi na usalama kwa watoto.
Maeneo hayo matano ya msisitizo katika utekelezaji wa programu hiyo, ni mwitikio wa Taifa katika utekelezaji wa malengo ya maeneleo endelevu ya Dunia –SDGs ambapo maeneo yote ya msisitizo ni utekelezaji wa malengo namba 2,3,4,na 16 ya SDGs.
Akizungumzia takwimu kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Mkurugenzi karia amesema Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa taarifa ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, inakadiriwa kuwa na jumla ya watu 936,302 ambapo wanaume ni 465,315, na wanawake ni 470, 987.
Kati ya watu wote hao, watu 199,697 sawa na asilimia 21% ni watoto wa umri wa chini ya miaka mitano (5).
Ambapo amesema takwimu hizo zinaashiria kuwa isipowekezwa kwenye malezi, makuzi na huduma sahihi kwa watoto basi Mkoa, Taifa na Bara la Afrika kwa ujumla litakabiliwa na changamoto kubwa ya kufikia maendeleo endelevu.
Hata hiyo ametoa rai kwa viongozi na wadau wakiwemo wa idara zote zinazotekeleza programu kuzingatia utekelezaji wa programu hiyo kwenye maeneo yao kupitia maelekezo na ushauri unaotolewa mara kwa mara.
Amewataka pia wakuu wa Taasisi na wadau wanaohusika na ulinzi na usalama wa mtoto kuweka mipangokazi ya kusaidia utengaji wa bajeti na kutoa fedha kwa utekelezaji.
Amewataka wadau wa vituo vya malezi kuhakikisha vinakuwa na madarasa yanayoongea, yaani madarasa ambayo yana vitendea kazi na vifaa yote ya kujifunzia kwa watoto wa awali.
Kwa upande wake Ummy Kileo, Afisa lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, amesema wataenda kusisitiza jamii kuzingatia lishe bora kwa mama mja mzito na hata baada ya mtoto kuzaliwa, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha mtoto kunyonyeshwa bila kula chochote kwa miezi sita.
Naye Afisa ustawi wa Jamii Jackson Chami amesema watoto wengi hawapati malezi bora ndani ya familia zao wawapo katika umri wa awali na kwamba changamoto kubwa ni kutokana na mifarakano ndani ya familia hivyo kupitia program hii, wazazi na walezi watapatiwa elimu ya namna ya kumuandaa mtoto ili kukabiliana na maisha yake ya baadae.
Mwalimu Pual Richard Magubiki ambae ni afisa Elimu Msingi, amesema katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna shule za Msingi 246, na kila shule ina wanafunzi wa darasa la awali.
Amesema elimu ya awali ndiyo inayohusika zaidi na program hiyo, kwasababu imejikita kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi miaka 8, na kuongeza kwamba amefurahishwa nayo kwakuwa wamekumbushwa kuwa ubongo wa mtoto unaimarika zaidi ndani ya miaka sifuri hadi sita ambao ndiyo umri wa mtoto wa darasa la awali.
Amesema kutokana na program hiyo anatarajia kwamba ikitekelezwa kikamilifu walimu watapokea watoto ambao ubongo wao umeimarika, wanajitambua na wanajua namna ya kuyatawala mazingira, jambo litakalowarahisishia walimu kuwafundisha stadi kuu tatu za kusoma kuhesabu na kuandika (KKK) kwasababu wazazi na walezi watakuwa wameshafanya kazi kubwa.
Ameongeza kutokana na program hiyo tayari Serikali kupitia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha Shilingi 587,000 kwa ajili ya kuweka vifaa kwenye madarasa 37 ya elimu ya awali na tayari vimeshatengenezwa kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri kwa watoto hao kujifunzia.
Programu hiyo ya miaka mitano ilianza mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wakiwemo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kama NELICO kwa upande wa Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa