Na, Agrey Singo.
Halmashauri ya wilaya Geita imekusanya mapato ya ndani jumla ya shilingi 6,274,151,382.98 ambayo ni sawa na makusanyo ya asilimia 122.6 ikiwa ni jumla ya mapato yote yaliyokusanywa katika vipindi vya robo zote 4 (Julai 2023 – Juni 2023) za mwaka wa fedha wa serikali 2022/2023.
Hayo yamebainishwa katika taarifa ya kamati ya kudumu ya fedha, uongozi na mipango kwa kipindi cha aprili hadi juni 2023, iliyowasilishwa katika mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani robo ya nne ya mwaka wa fedha 2022/2023, kilichofanyika Julai 28, 2023 kwa ajili ya kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za serikali ngazi ya halmashauri katika robo ya nne ya mwaka huo wa fedha.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi kufikia mwezi Juni 2023, Halmashauri ya wilaya Geita ilikusanya kiasi cha shilingi 704,307,738.53 ikiwa ni mapato fungwa sawa na asilimia 120.62 ya makisio na shilingi 5,569,843,644.45 ikiwa ni mapato yasiyofungwa sawa na asilimia 122.36, ambayo imepelekea jumla mapato ya ndani kufikia shilingi 6,274,151,382.98 ambayo ni sawa na makusanyo ya asilimia 122.6.
Katika mapato hayo kiasi cha shilingi 1,820,802,623.60 kilihamishwa kwenda akaunti ya maendeleo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha, kufikia mwezi Juni 2023, halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi 1,368,560,056 fedha za sequip kwa kwa kata za Isulwabutundwe na Ludete kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za watumishi na shule mbili mpya.
Sambamba na hilo, taarifa hiyo imeongeza kuwa kufikia mwezi Juni 2023, halmashauri ya wilaya ya Geita ilipokea jumla ya shilingi 47,943,924,716.00 ikiwa ni ruzuku ya mishahara sawa na asilimia 76.60, shilingi 1,434,024,500.00 ikiwa niruzuku ya matumizi mengineyo sawa na silimia 110.07 ya makisio, shilingi 15,017,804,999.17 ikiwa ni ruzuku ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 94.4 na shilingi 11.131,720,282.15 ilipokelewa nje ya bajeti.
Hivyo, jumla ya mapato yote yaliyopokelewa au kukusanywa ni shilingi 81,799,504,890.27 ambayo ni sawa na asilimia 96.52 ya makisio ya mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Akizungumza katika mkutano huo wa baraza la madiwani robo ya nne ya mwaka wa fedha 2022/2023, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Mhe. Charles Kazungu amewapongeza waheshimiwa madiwani pamoja na watumishi wote wa halmashauri kwa usimamzi na ufuatiliaji uliopelekea kufikia mafanikio hayo makubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Geita, Ndugu Karia Rajabu Magaro amewataka waheshimiwa madiwani na watendaji wa serikali kuzidisha ushirikiano ili kuendelea kufuatilia na kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao pamoja na suala la ukusanyaji wa mapato.
Naye, mkuu wa wilaya Geita, Mhe. Cornel Magembe ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Geita kwa kufikia mafanikio hayo ya kukusanya mapato ya ndani kwa kuvuka lengo na kufikia asilimia 122.6 kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikianoa kwa mwaka mpya wa fedha wa 2023/2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa