Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo ametoa wito wa kuwataka wanachi wanaofanya biashara katika masoko mbalimbali kuchukua tahadhari za kukabiliana na ajali za moto kwa kuboresha miundo mbinu na kutokutumia vyanzo hatarishi vya moto katika mazingira hayo.
Ameyasema hayo Januari 27 alipoambatana na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Geita pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la CCM Kakubilo walipokwenda kuangalia athari za ajali ya moto uliotokea usiku wa Januari 25 na kuteketeza vibanda 16 vya biashara katika soko hilo.
Mhe.Shimo amesema kuwa ubora wa miundo mbinu katika masoko unaweza kusaidia kudhibiti athari zaidi pale ajali ya moto inapotokea kwa kuwa magari ya zimamoto yanaweza kufika na kuingia kona zote kwa urahisi huku akimtaka Mkuu wa jeshi la polisi Wilaya kuwatafuta watu waliohusika kuiba baadhi ya bidhaa za wafanyabiashara wakati wa ajali hiyo huku akikemea vikali tabia za kuiba mali za watu pindi yanapotokea majanga.
Naye Mkuu wa jeshi la zimamoto Wilaya ya Geita Inspekta Stanley Lwago amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kuchukua tahadhari za moto kwa kutenganisha maeneo ya kufanyia biashara na shughuli za mapishi, kuwa na vifaa vya kuzimia moto, na hata kufunga vifaa maalumu vya kung’amua moto majumbani na sehemu za biashara vinavyotoa taarifa ya moto ukiwa katika hatua ya chini kabisa baada ya kuhisi moshi, huku akishauri kupishanisha kuta zinazotenganisha vyumba ili kuzuia moto kuhamia chumba kingine kwa urahisi.
Awali mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe.Charles Kazungu licha ya kutoa pole kwa wahanga hao amemuomba Mkuu wa Wilaya kusaidia kuangalia njia mbadala ya kuwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupata angalau magari mawili ya zimamoto ya kuazia hata kama ni kwa kupitia fedha za CSR ili kusaidia katika kukabiliana na majanga ya moto katika tarafa za Busanda na Bugando.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga awali akitoa taarifa kwa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 25 majira ya saa mbili kasorobo usiku huku akiwashukuru wananchi ambao walishiriki kuuzima moto huo ambao umeleta madhara ya kuunguza mali pekee bila madhara kwa binadamu.
Baadhi ya Wahanga wa ajali hiyo ya moto akiwemo Bw.Renatus Elias aliyekuwa na duka la nguo amesema kuwa ajali hiyo imeathiri mtaji wake kwa kuwa mali yenye thamani ya shilingi milioni 8 imeteketea kwa kuungua na baadhi ya mali kuibiwa na watu wasio na nia njema wakati alipokuwa akijaribu kuokoa mali zake usiku huo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa