Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amesema, kilimo cha mazoea ndiyo kikwazo cha maendeleo ya zao la pamba ambapo amewataka wakulima kubadilika na kuanza kulima kisasa ili waweze kupiga hatua.
Shimo alisema hayo Februari 25, 2022 katika vijiji vya Bufunda, Nyakasalala na Chigunga Wilayani Geita wakati akikagua mwenendo wa kilimo cha pamba kwa wakulima na Vyama vya Ushirika (AMCOS).
Alisema bado wakulima wengi wanapanda kwa mazoea na kutozingatia kanuni za matumizi sahihi ya dawa na mbolea ndiyo maana kilimo cha zao hilo kimeendelea kudidimia kila uchwao.
Alishauri, iwapo wakulima wa pamba watalima kulingana na maelekezo ya wataalamu itawasaidia kukabiliana na wadudu na kuongeza mavuno hadi Kilo 1000 kwa hekari na kujiongezea kipato.
Shimo aliwataka viongozi wa Amcos zote wilayani Geita kuendelea kuwa mfano kwa kulima mashamba darasa yatakayowasaidia wakulima kujifunza kwa vitendo na Amcos zenyewe kujipatia kipato.
Afisa Kilimo kutoka Bodi ya Pamba wilayani Geita, Ndida Anthony alieleza, msimu huu wamebaini asilimia 40 ya wakulima wamelima pamba kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora na asilimia 60 wakiwa wamelima kwa mazoea.
“Changmoto kubwa wakulima wengi kutofuata kanuni za kilimo hawatumii mbolea, wamelima tu, lakini changamoto nyingine ambayo inaumiza vichwa ni wakulima kuendelea kuchanganya pamba na mazao mengine,”
Mkulima wa Pamba katika kijiji cha Bufunda, Matulanya Masala alisema changamoto kubwa ni kuadimika kwa viuatilifu na pampu za kupulizia dawa hivyo kuiomba bodi ya pamba kuwasogezea huduma hizo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa