Na. Michael Kashinde
Wito umetolewa kwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambao ndio wenyeviti wa kamati za maendeleo ya kata kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha zilizotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Ujenzi wa miundombinu ya Elimu ili fedha hizo zikamilishe kazi hizo kwa ubora na kiwango kilichokusudiwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu ametoa wito huo wakati akihitimisha mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani wa Robo ya Tatu kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mei 04, 2023 katika ukumbi wa Halmashauri Nzera, ambapo amewataka madiwani hao kuzisimamia kamati za maendeleo katika kata zao ili fedha hizo zinazoingizwa kwenye akaunti za shule zifanye kazi iliyolengwa na Mhe. Rais.
Mhe. Kazungu ametumia mkutano huo wa baraza la madiwani kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Geita kiasi cha Tshs. 1, 891, 500, 000/= kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule kupitia Mradi wa BOOST, pamoja na kiasi cha Tshs. 1, 788, 250, 000/= ambazo ni fedha kutoka Serikali kuu.
Aidha baraza hilo kupitia Mwenyekiti wake Mhe. Charles Kazungu limeishukuru pia Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya BARRICK kwa kutoa ufadhili wa kiasi cha Tshs. 487, 300, 000/= katika sekta ya Elimu kwa ajili ya ujenzi wa Miundombinu ya shule za kidato cha Tano na Sita huku madiwani wakishauriwa kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyia kazi watumishi mbalimbali hasa wa idara ya Elimu ili kuongeza ufaulu zaidi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita Ndugu Barnabas Mapande akizungumza katika mkutano huo wa baraza la madiwani ameanza kwa kushukuru kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo kwa kipindi kifupi cha miaka miwili tu, ametoa fedha za kujenga shule nyingi ambazo idadi yake inakaribia idadi ya shule zote zilizokuwepo miaka yote ya nyuma huku zikiwa na ubora wa hali ya juu.
Aidha ametoa ushauri kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuzikarabati shule ambazo zinaonekana kuchakaa ili ziweze kukaribia au kufananafanana na zile zilizojengwa kwa fedha za Mhe. Rais, huku akisisitiza usawa wa walimu katika maeneo yote, licha ya tofauti za kimazingira suala linalopelekea baadhi ya maeneo kukimbiliwa na mengine kukimbiwa na walimu hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Adv. John Paul Wanga akizungumza katika baraza hilo la madiwani ameeleza kuwa Halmashauri ina mpango wa kushirikiana na wananchi kuboresha mazingira ya watumishi hasa walimu katika maeneo ya nje ya mji kwa kuwajengea nyumba na kuwapatia samani za ndani ikiwa ni sehemu ya motisha kwao ili waweze kuishi kwa furaha katika mazingira hayo.
Akizungumzia huduma ya matibabu bure kwa wazee Adv. Wanga amelieleza baraza la madiwani kuwa Halmashauri imetoa maelekezo kwa watendaji wa kata zote kubaini na kuwatambua wazee wasio na uwezo, ili kuwaweka katika mpango huo wa kupata matibabu bure ambapo lengo la kuwatambua ni kuwapata wale ambao kweli wanauhitaji huo na hawana uwezo.
Mkutano huo wa baraza la madiwani Kwa kipindi cha robo ya Tatu kwa mwaka wa fedha 2022/2023 umejadili na kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za kiserikali ngazi ya Halmashauri kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2023 ambapo baraza hilo limeazimia masuala mbalimbali ikiwemo kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa