Na. Michael Kashinde
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Ndg. Barnabas Mapande amewataka wananchi wa Wilaya hIiyo kuendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Wilaya ya Geita kiasi cha bilioni 6.78 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya kisasa ya elimu ya sekondari yakiwa na viti vyake jambo ambalo halikuwahi kutokea hapo awali.
Mapande ameyasema hayo Novemba 8, 2021 akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita katika Shule ya Sekondari Inyala ambapo kuna mradi wa vyumba 11 vya madarasa, wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuangalia hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa madarasa hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Amesema kuwa hapo awali mwanafunzi alikuwa akichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza alitakiwa kununua kiti na meza kwa ajili ya kutumia shuleni, jambo ambalo kwa sasa halitakuwepo, kwa kuwa mwanafunzi atakuta kiti na meza shuleni suala ambalo limewapunguzia wazazi mzigo mkubwa, huku akisisitiza kuwa huo ni upendo wa hali ya juu wa Mhe. Rais ambaye ni Mama kwa watoto wa Geita na Tanzania kwa ujumla.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Inyala, Mapande ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa namna inavyosimamia ujenzi wa madarasa hayo kwa ubora unaotakiwa, huku akiwataka wahandisi wa miradi hiyo kufuatilia kwa karibu na kuongeza kasi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati, ambapo pia amewahamasisha wananchi kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kujitolea nguvu zao katika miradi hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo akiwa katika ziara hiyo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita na wananchi kwa ujumla kwa kuwa na wazo la kuanzisha shule mpya kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika badala ya kuongeza tu madarasa katika shule zilizopo, kwa kuwa jambo hilo la kuanzisha shule mpya litawapunguzia wanafunzi hao adha ya kusafiri umbali mrefu kila siku kwenda shuleni.
Mheshimiwa Shimo ametoa rai kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ambapo kuna ujenzi wa shule mpya za Sekondari, kuhakikisha wanajipanga na kujenga ofisi za walimu badala ya kutumia madarasa kama ofisi, huku akifafanua kuwa madarasa mengi yanajengwa ila yanapokatwa mengine ili kutumika kama ofisi idadi ya madarasa inapungua, lakini pia si haki na hadhi ya mwalimu kutumia darasa kama ofisi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Khadija Said Joseph ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoangalia mahitaji ya watanzania na kuyatekeleza, ambapo ameipatia Halmashauri ya Wilaya ya Geita kiasi cha Shilingi Bilioni 5.34 kwa ajili ya vyumba 267 vya madarasa ya Sekondari, huku akiahidi kupokea ushauri mbalimbali uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo na kuufanyia kazi ili kujenga madarasa bora na kuyakamilisha kwa wakati.
Kupitia fedha hizo za ujenzi wa madarasa ya shule za Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeazimia kuanzisha shule mpya 22 badala ya kujenga vyumba vya madarasa katika shule 39 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wingi wa wanafunzi, umbali mrefu kwenda shuleni, utoro wa muda mrefu kwa wanafunzi, uwepo wa maeneo ya ujenzi wa shule mpya na baadhi ya maeneo kuwa tayari yameanzisha ujenzi wa shule kabla ya ujio wa fedha hizo.
Kamati ya Siasa Wilaya ya Geita imetembelea na kukagua mradi wa vyumba 11 vya madarasa katika shule ya sekondari Inyala, vyumba 19 vya madarasa katika shule ya sekondari Nyawilimilwa, vyumba 9 vya madarasa katika shule ya sekondari Senga, vyumba 11 vya madarasa katika shule ya sekondari Nyabalasana na vyumba 7 vya madarasa katika shule ya sekondari Igate ambapo Kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi wa madarasa hayo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa