Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa Serikali za mitaa ngazi ya vijiji wapatao 145 wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wameapishwa leo Oktoba 2, 2024.
Uapisho huo umeongozwa na Muchunguzi Mujuni Sailous Hakimu Mkazi Mwandamizi katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita zamani-Bomani.
Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Vijiji Wakiapa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Muchunguzi Sailous Leo Oktoba 2, 2024 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita zamani-Bomani
Pamoja na zoezi la kuapishwa, wasimamizi wasaidizi hao wamepewa mafunzo kuhusu namna watakavyotekeleza majukumu yao kabla, wakati na baada ya zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika ufafanuzi wake kwa wasimamizi Wasaidizi hao, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Amina Sungura amesema zoezi hilo linaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji na vitongoji katika Mamlaka ya Wilaya ya Mwaka 2024.
Amewataka wasimamizi kuzingatia muongo katika kazi yao ikiwemo kutokuwa viongozi wa vyama vya siasa, kuwa Watiifu na Waadilifu, Waaminifu na kutunza siri.
Pichani wa kwanza Kushoto ni Mwanasheria Amina Sungura, Aliyekaa katikati ni Afisa Msimamizi Msaidizi Jonas Kilave na wa kwanza kulia ni Afisa Msimamizi Msaidizi Sarah Yohana ngazi ya Halmashauri
Kuhusu sifa za mpiga kura Mwanasheria Sungura, amesema kuwa mpiga kura lazima awe Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, awe mkazi wa mtaa,kijiji au kitongoji anapoishi, awe na akili timamu na awe amejiandikisha katika kitabu cha mpiga kura katika mtaa,kijiji au kitongoji husika.
Naye Afisa Msimamizi msaidizi Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi Sarah Yohana amewataka wasimamizi wasaidizi kuwa makini na zoezi hilo kwa kuwa wamepewa dhamana ya kufanya kazi hiyo kwasababu wameaminiwa hivyo wafanye kazi na kuikamilisha kama ilivyokusudiwa.
Afisa Msimamizi Msaidizi Bi. Sarah Yohana akitoa maelekezo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Vijiji katika mafunzo yaliyofanyika Bomani Geita Mjini Leo Oktoba 2, 2024.
Akihitimisha mafunzo hayo Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg Karia Rajabu Magaro amewatangazia wasimamizi wasaidizi kwamba tarehe ya uandikishaji wapiga kura ni Oktoba 11 hadi 20, 2024 hivyo wahakikishe kwamba unafanyika kama unavyostahili.
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndugu Karia Rajabu Magaro akitoa maelekezo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Vijiji katika Ukumbi wa Mikutano Bomani Geita Mjini Leo Oktoba 2, 2024
Amewataka wasimaizi wasaidizi kudumu katika maeneo yao ya kazi na kwamba kama kuna sintofahamu yoyote wanapaswa kutoa taarifa kwa Afisa uchaguzi au Msimamizi wa Uchaguzi.
Amesema pia hatosita kumchukulia hatua msimamizi msaidizi ngazi ya kijiji yeyote atakaeshindwa kutekeleza wajibu wake vizuri hivyo kila mmoja afanye kazi hiyo kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.
Lameck Warioba msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambaye ni Afisa mtendaji kijiji cha Ikina kata ya Bukoli Wilaya ya Geita, amesema amepokea mafunzo hayo kwa umakini na anaahidi kwenda kusimamia zoezi hilo kwa haki na kwa kuzingatia misingi, kanuni na taratibu zilizotolewa.
Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Vijiji wakijaza fomu za viapo Oktoba 2, 2024 kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa